Kuhusu kampeni

Tunacholenga kufanikisha kupitia kampeni hii

Kampeni hii inalenga kusaidia watu kuelewa vyema maana ya mpango wa afya kwa wote – waelewe ni huduma zipi na usaidizi upi unaostahili kuwepo na mahali gani pa kuzipata. Tutatoa maelezo ya picha/michoro/video ambayo husaidia watu wenye uwezo wa kufikia huduma bora za afya, na za gharama nafuu kuelewa jinsi maisha yalivyo kwa watu wasioweza kuzifikia huduma hizo, na hivyo basi kutetea upatikanaji sawa wa huduma hizo kila mahali.

Wahudumu wa afya watakuwa na wajibu muhimu wa kuchangia katika kampeni hii, wakisaidia wenye jukumu la kufanya maamuzi kuhusu afya, watambue kile wanachohitaji wanajamii kuhusiana na tiba, hasa katika ngazi ya huduma za kimsingi.

Kampeni hii pia inawapa nafasi mawaziri wa afya na maafisa wengine wa serikali wanaofanya maamuzi kujitolea kuchukua hatua ya kuziba mapengo yaliyopo katika mpango wa huduma za afya kwa wote katika nchi zao, pamoja na kubainisha hatua ambazo tayari zimepatikana.

Kuhusu Siku ya Afya Ulimwenguni, tutatoa chapisho la kila mwaka la WHO la data ya afya, Ripoti ya Takwimu za Afya Ulimwenguni. Ripoti hiyo itajumuisha habari kuhusu mielekeo ya afya katika fani fulani maalum kama vile afya ya watoto wachanga na watoto wote, maradhi yasiyo ya kuambukiza, afya ya akili na hatari za kimazingira, na pia data kuhusu mpango wa afya kwa wote na mifumo ya afya.

Mpango  wa afya kwa wote- taswira pana

Siku ya Afya Ulimwenguni 2019 inaadhimishwa katikati ya kufanyika kwa Kongamano la Kimataifa kuhusu Huduma za Afya za Kimsingi lililofanyika jijini Astana, Kazakhstan mnamo Oktoba 2018 na Mkutano wa Ngazi za Juu kuhusu afya kwa wote kwenye Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Septemba 2019. Siku hiyo ni mojawapo ya nafasi nyingi za kuzungumzia umuhimu wa usawa katika huduma za afya, si tu kwa afya ya watu binafsi bali pia kwa afya ya mataifa na jamii kwa jumla.