Maelezo muhimu ya hali
- Angaa nusu ya idadi ya watu ulimwenguni bado hawawezi kupata huduma muhimu za afya.
- Takriban watu milioni 100 bado wanaendelea kusukumwa katika umaskini mkubwa (yaani wanaishi kwa Dola 1.90 au chini yake kwa siku) kwa sababu wanalazimika kulipia huduma za afya.
- Watu zaidi ya milioni 800 (karibu 12% ya idadi ya watu ulimwenguni) walitumia angalau 10% ya bajeti zao za nyumbani kulipia matibabu.
- Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekubali kujaribu kufaulisha mpango wa afya kwa wote (UHC) kufikia 2030, kama sehemu ya Malengo ya Ustawi Endelevu.
UHC ni nini?
UHC inamaanisha kuwa watu wote na jamii wanapokea huduma za matibabu wanazohitaji bila kutatizika kifedha. Hii inajumuisha upeo mzima wa huduma za kimsingi na bora za afya kuanzia mahimizo ya afya hadi katika uzuiaji, matibabu, huduma za urekebishaji na ushauri kuhusu magonjwa yasiyopona.
UHC inawezesha kila mmoja kupata huduma zinazohusiana na sababu kuu za chanzo cha maradhi na vifo, na kuhakikisha kuwa ubora wa huduma hizo unafaa kuimarisha afya ya watu wanaozipokea.
Kuwalinda watu na athari za kulipia huduma za afya kutoka kwa mifuko yao hupunguza hatari ya watu kusukumwa katika umaskini kwa sababu maradhi yanayotarajiwa huwahitaji kutumia akiba yao, kuuza mali, au kukopa- hivyo basi kuharibu mustakabali wao na hata wa watoto wao.
Kufaulisha mpango wa UHC ni mojawapo ya malengo yaliyowekwa na mataifa ya ulimwengu yalipokubali Malengo ya Ustawi Endelevu mnamo 2015. Nchi ambazo zimepiga hatua katika UHC zitapiga hatua pia katika mambo mengine yanayohusiana na afya, na kata malengo mengineyo. Afya njema huwezesha watoto kusoma na watu wazima kujipa mapato, husaidia watu kukwepa umaskini, na kutoa msingi wa maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu.
UHC sio
Kuna mambo mengi ambayo hayajajumuishwa katika upeo wa UHC:
- UHC haimaanishi huduma bila malipo kwa aina zote za matibabu, bila kuzingatia gharama, kwa kuwa hakuna nchi inayoweza kutoa huduma zote bila malipo na kudumisha hilo kwa muda mrefu.
- UHC haihusu tu ufadhili wa afya. Inajumuisha masuala yote ya mfumo wa afya: mifumo ya utoaji huduma za afya, wahudumu wa afya, vituo vya afya, mifumo ya mawasiliano, teknolojia za afya, mifumo ya habari, mbinu za kuhakikisha ubora, na uongozi na sheria.
- UHC haihusu tu kuhakikisha kiwango cha chini cha huduma za afya, lakini pia kuhakikisha kuwa huduma hizo zinapanuliwa taratibu na kinga ya kifedha kadri rasilmali zaidi zinavyopatikana.
- UHC haihusu tu huduma za matibabu ya mtu binafsi, bali inajumuisha huduma zinazolenga jamii kama vile kampeni za afya ya umma, kuongeza dawa ya fluoride katika maji, kudhibiti maeneo ya mbu kuzaana, na mengine zaidi.
- UHC inajumuisha mambo zaidi ya afya; kuanza kupiga hatua zinazohusu UHC kunamaanisha hatua zinazoelekea kwenye usawa, maendeleo muhimu, na ujumuishaji na uwiano wa kijamii.
Nchi zinaweza kupiga vipi hatua katika UHC?
Nchi nyingi tayari zinapiga hatua kufikia UHC. Nchi zote zinaweza kuamua kupiga hatua za upesi au kudumisha mafanikio ambayo tayari zimepata. Katika nchi ambapo huduma za afya kwa kawaida zimekuwa zikipatikana na kwa gharama nafuu, serikali zinaendelea kukabiliana na changamoto za kushughulikia mahitaji ya afya yanayozidi kuongezeka ya wananchi na gharama zinazoongezeka za huduma za afya.
Kuelekea kufaulisha UHC kunahitaji kuimarisha mifumo ya afya katika nchi zote. Miongozo thabiti ya ufadhili ni muhimu. Watu wanapohitajika kulipia nyingi ya gharama za huduma za afya kutoka mifukoni mwao, maskini mara nyingi hushindwa kupata nyingi ya huduma wanazohitaji, na hata wanaojiweza huenda wakapata ugumu wa kifedha iwapo magonjwa yatazidi au magonjwa hayo yatakaa kwa muda mrefu kabla ya kupona. Kukusanya pesa kutoka kwa vyanzo vya kimsingi vya ufadhili (kama vile michango ya lazima ya bima) inaweza kusambaza hatari za kifedha zinazotokana na maradhi kwa watu wengi.
Kuimarisha kuwepo kwa huduma za afya na matokeo ya afya hutegemea uwepo, ufikiaji na uwezo wa wahudumu wa afya kutoa huduma bora za pamoja zinazoegemea kwa watu. Uwekezaji katika huduma bora za afya za kimsingi utakuwa njia kuu ya kufaulisha UHC kote ulimwenguni. Kuwekeza katika wahudumu wa mpango wa afya ya kimsingi ni njia yenye gharama nafuu zaidi ya kuhakikisha huduma muhimu zimeimarika. Uongozi bora, mifumo thabiti ya uagizaji na usambazaji dawa na teknolojia za afya pamoja na mifumo inayofanya kazi ya habari kuhusu afya ni masuala mengine muhimu zaidi.
Huduma ya afya ya kimsingi ni nini?
Huduma ya afya ya kimsingi ni njia ya kufanikisha afya na uzima inayoegemea kwa mahitaji na hali za watu binafsi, familia na jamii. Inashughulikia kwa kina masuala ya afya na uzima wa viungo, akili na jamii.
Inahusu kutoa huduma zote za matibabu anazohitaji mtu katika kipindi chote cha maisha yake, na sio kutibu maradhi fulani pekee. Huduma ya afya ya kimsingi huhakikisha watu wanapokea huduma kamili, zinazojumuisha mahimizo, kuzuia na matibabu, huduma za urekebishaji na kutoa ushauri kwa wagonjwa wasioweza kupona na kuhakikisha kuwa watu wanazipata katika mazingira ya maisha ya kila siku.
WHO imebuni fasili linganifu ya afya ya kimsingi kwa kuzingatia masuala matatu:
- Kuhakikisha kuwa matatizo ya kiafya ya watu yanashughulikiwa kupitia njia ya mahimizo, kulinda, kuzuia, kutibu, kurekebisha na ushauri kwa magonjwa yasiyopona katika kipindi chote cha maisha huku umuhimu ukipewa majukumu muhimu ya kimfumo yanayolenga watu binafsi na familia na wanachi kama wahusika wakuu katika utoaji wa huduma jumuishi katika ngazi zote za huduma;
- Kushughulikia vielelezo vikuu vya afya (ambavyo ni kijamii, kiuchumi, kimazingira, pamoja na desturi na mienendo ya watu) kupitia sera thibitifu zilizoshirikisha umma na hatua zinazochukuliwa katika sekta zote; na
- Kuhamasisha watu binafsi, familia, na jamii kuimarisha afya zao, kama watetezi wa sera ambazo zinahimiza na kulinda afya na uzima, kama washirika katika huduma za afya na za kijamii kupitia kushiriki kwao, na kama wanaojitunza kibinafsi na kuwatunza wenzao.
Huduma ya afya ya kimsingi ni njia faafu zaidi na yenye gharama nafuu ya kufaulisha mpango wa afya kwa wote kote ulimwenguni.
Kutimiza mahitaji ya wahudumu wa afya ya Malengo ya Ustawi Endelevu na huduma za afya kwa wote, wahudumu wa afya wa ziada wanaozidi milioni 18 wanahitajika kufikia 2030. Mapengo katika usambazaji na hitaji la wahudumu wa afya yanapatikana zaidi katika nchi zenye mapato ya chini na kadri. Ongezeko la hitaji la wahudumu wa afya linakadiriwa kuongeza takribani nafasi milioni 40 za kazi katika sekta ya afya kwenye uchumi wa ulimwengu kufikia 2030. Uwekezaji unahitajika kutoka kwa sekta za umma na pia kibinafsi katika elimu ya wahudumu wa afya, pamoja na kuunda na kujaza nafasi zinazofadhiliwa katika sekta ya afya na uchumi wake.
UHC haisisitizi tu kuhusu ni huduma zipi zinazojumuishwa, bali pia jinsi zinavyofadhiliwa, kusimamiwa na kutekelezwa. Mabadiliko makuu katika utoaji huduma yanahitajika ili huduma hizo ziwe jumuishi na zinazoangazia mahitaji ya watu na jamii. Hii inajumuisha kuzielekeza upya huduma za afya ili kuhakikisha kuwa zinatolewa katika mazingira yanayofaa zaidi, na pia kuwianisha huduma za wanaotibiwa na kuondoka na wanaolazwa, na kuimarisha uratibu wa huduma. Huduma za afya, ambazo ni pamoja na matibabu ya dawa za kienyeji na za kisasa, zikiratibiwa kwa kuegemea mahitaji kamili na matarajio ya watu na jamii zitasaidia kuhamasisha na kuwafanya kujihusisha zaidi katika afya yao na mfumo wa afya.
UHC inaweza kutathminiwa?
Ndiyo. Kufuatilia hatua zilizopigwa katika kufanikisha UHC kunafaa kuzingatia mambo mawili:
- Idadi ya watu wanaoweza kupata huduma bora muhimu za afya.
- Idadi ya watu wanaotumia kiasi kikubwa cha mapato yao kwa afya.
Pamoja na Benki ya Dunia, WHO imeunda utaratibu wa kufuatilia hatua ilizopiga UHC kwa kufuatilia vitengo vyote viwili, na kwa kuzingatia ngazi zote za jumla na kiwango cha usawa ambacho UHC inaweza kufikia, kutoa huduma na kuhakikisha ipo kinga ya kifedha kwa watu wote walio mahali fulani, kama maskini au wanaoishi maeneo ya mashambani.
WHO hutumia huduma 16 muhimu za afya katika vitengo 4 kama vigezo vya ngazi na usawa wa utoaji huduma katika mataifa:
Afya ya uzazi, ya mjamzito, ya watoto wachanga na ya watoto:
- Mpango wa uzazi
- Kliniki ya wajawazito na huduma za kujifungua
- chanjo kamili ya mtoto
- mienendo ya kutafuta tiba ya homa ya mapafu(nimonia)
Maradhi ya kuambukiza:
- matibabu ya kifua kikuu
- Matibabu ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (HIV)
- Matibabu ya Homa ya Ini (Hepatitis)
- Utumizi wa vyandarua vyenye dawa kuzuia malaria
- Usafi wa hali ya juu
Maradhi yasiyo ya kuambukiza:
- kuzuia na kutibu shinikizo la damu
- kuzuia na kutibu kupanda kwa sukari mwilini
- kuchunguza saratani ya mlango wa uzazi
- Tumbaku (kwa wasiovuta)
Uwezo wa huduma na upatikanaji wake:
- kufikia huduma za kimsingi hospitalini
- idadi ya wahudumu wa afya
- upataji wa dawa muhimu
- Usalama wa kiafya: kutimiza Kanuni za Kimataifa za Afya.
Kila nchi ina upekee wake, na kila nchi huenda iangazie fani tofauti au kubuni njia zao za kupima ufanisi wa UHC. Lakini pia kuna thamani katika mbinu ya kimataifa ambayo hutumia vigezo sanifu ambavyo vinatambuliwa kimataifa ili ufanisi huo uweze kulinganishwa kimataifa na kwa muda mrefu.
Wajibu wa WHO
UHC imejikita katika Katiba ya WHO ya 1948, ambayo inashikilia kuwa afya ni haki muhimu ya binadamu na inajitolea kuhakikisha viwango vya juu zaidi vya afya kwa wote.
WHO inasaidia mataifa kuunda mifumo yao ya afya Ili kuelekea kufanikisha UHC, mbali na kufuatilia hatua zilizopigwa. Lakini WHO haiko pekee yake: WHO inafanya kazi na washirika wengi tofauti katika hali tofauti kwa madhumuni tofauti ya kuendeleza UHC kote ulimwenguni.
Baadhi ya washirika wa WHO ni pamoja na:
- UHC2030
- Alliance for Health Policy and Systems Research
- P4H Social Health Protection Network
- European Union-Luxembourg-WHO Partnership for UHC
- Primary Health-Care Performance Initiative
Mnamo Oktoba 25-26, 2018, WHO kwa ushirikiano na UNICEF na Wizara ya Afya ya Kazakhstan iliandaa Kongamano la Ulimwengu kuhusu Huduma za Afya ya Kimsingi, miaka 40 baada ya kuidhinisha Azimio la kihistoria la Alma-Ata. Mawaziri, wahudumu wa afya, wasomi, washirika na mashirika ya kijamii waliungana kujitolea upya kufanikisha huduma za afya za kimsingi kama msingi imara wa UHC katika Azimio jipya la Astana (Declaration of Astana). Azimio hilo linalenga kuzindua upya kujitolea kisiasa kwa huduma za afya za kimsingi kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo kiserikali, makundi ya wataalam, wasomi na mashirika ya afya na maendeleo ulimwenguni.
Nchi zote zinaweza kufanya zaidi katika kuimarisha matokeo ya kiafya na kushughulikia umaskini, kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, na kwa kupunguza umaskini unaohusishwa na ulipiaji wa huduma za afya.